Jinsi ya kufuga ng'ombe wa maziwa katika shamba dogo - Dar East Project

Post Top Ad

Jinsi ya kufuga ng'ombe wa maziwa katika shamba dogo

Jinsi ya kufuga ng'ombe wa maziwa katika shamba dogo

Share This
BAADHI ya wafugaji wa ng'ombe hudhani kufuga kwa ajili ya maziwa huwa ni ghali sana kuwalea, hasa wengi wakidhani sharti ng'ombe hao wawe katika mashamba makubwa.

Hivyo basi, unagundua uzalishaji wa maziwa nchini Kenya ungali chini na kusababisha bei ya bidhaa hiyo kuwa ghali. Maziwa ni kiungo muhimu kwa binadamu ikizingatiwa kuwa kando na mayai na nyama, bidhaa hiyo pia ina ukwasi wa madini ya Protini.

Wakulima wachache nchini ndio wamekumbatia ufugaji wa ng'ombe wa maziwa, na la kutia moyo wengi wao hawana mashamba makubwa inavyodhaniwa.

Mataifa kama vile; India, Brazil, China na Marekani ndio bora katika ufugaji wa ng'ombe wa maziwa duniani. Aidha, mataifa hayo yamekumbatia mfumo wa teknolojia ya kisasa kufuga ng'ombe, hasa katika kukama maziwa.

Aina ya ng'ombe wanaotambulika kwa uzalishaji mkubwa wa maziwa ni; Ayrshire, Jersey, na Friesian. 

Nchini Kenya wengi wa wafugaji wa ng'ombe huwafuga kwa minajili ya nyama na kuwauza kwa ajili ya mapato, hususan jamii za kuhamahama kuwatafutia mifugo.

Wachache wanaofuga ng'ombe kwa minajili ya maziwa wanaeleza kuwa si lazima mfugaji awe na shamba kubwa kuafikia ufugaji huo. Bw Mwae Malibet ni mfugaji wa ng'ombe wa maziwa aina ya Fresian Gachie kaunti ya Kiambu, na anafichua kuwa ana kipande kidogo cha ardhi kuendesha azma yake.

"Shamba langu ni nusu ekari pekee, na ndilo nimefugia ng'ombe mbali na kukuza mimea mbalimbali," aeleza.

Kando na ng'ombe, Malibet hukuza mboga kama vile; Spinachi, Sukuma wiki, Kabichi na za kienyeji ja; managu na terere, ikiwa ni pamoja na nyanya na hoho kwenye mahema 'Greenhouse'.

Shamba hilo, ameligawanya kiasi kwamba limetoshea shughuli zote hizo. Zizi la ng'ombe lina ukubwa wa 20 kwa 50. Ana ng'ombe watatu wa maziwa anaokama.

Mkulima huyo anashauri kwamba la muhimu ni kuzingatia lishe kwa wanyama hao, pamoja na matibabu yake. "Hayo yote huafikiwa kwa kuzingatia kiwango cha usafi," asema.

Wengi hujisumbua kuwa ng'ombe huhitaji majani mabichi kuwafuga, lakini kwake la hasha. Badala yake anaeleza kwamba ufugaji mwema wa mifugo ni kwa kutumia lishe iliyokauka.

Nyasi zilizokauka aina ya 'hey', chakula maalum cha ng'ombe kilichosagwa kutokana na nafaka ndicho chakula anachotumia kuwalisha. "Ninapowalisha majani, huhakikisha yamekauka kabisa," adokeza Bw Malibet.

Mtaalamu wa kilimo na ufugaji kaunti ya Nairobi Bi Veronicah Kirogo ameeleza Swahilihub kwamba kiukulima na ufugaji, lishe iliyokauka  ndiyo hupendekezwa kwa kuwa haina athari zozote kwa mifugo.

"Mifugo wowote wale wanafaa kulishwa chakula kilichokauka, kama vile nyasi (hay) ambazo zimekauka, chakula kilichosagwa kutoka kwa nafaka huwa kimekauka. Chakula hicho hakuna wadudu kamwe. Vilevile, hufanya mifugo wanywe maji kwa wingi yanayosaidia chakula chenyewe kusagika upesi," ashauri Bi Kirogo.

Mtaalamu huyo anaendelea kushauri kuwa ni vyema chakula kinacholishwa mifugo kizingatie usawa wa madini mfano; Protini, Vitamini, Wanga, Kalsiamu, Potasiamu na madini mengineyo muhimu kwa miili ya mifugo.

Chakula chenye Legumes kwa ng'ombe pia mtaalamu huyo anashauri kulishwa kwao. Legumes huwa kwenye nafaka kama vile; maharage, njugu, kunde, miongoni mwa zingine.

Bw Stephene Mathenge ni mfugaji mwingine anayefuga ng'ombe wa aina ya; Ayrshire, Jersey, na Friesian Kiangai kaunti ya Kirinyaga.

Aidha, mfugaji huyo ana zaidi ya ng'ombe 10 wa maziwa.

Kauli yake kuhusu ufugaji wa ng'ombe wa maziwa inaenda sawia na ya Bw Mwae Malibet wa Gachie Kiambu.

Bw Mathenge pia hana kipande kikubwa cha shamba, japo zizi la ng'ombe wake limejengwa katika takriban robo ekari ya shamba hilo. Alieleza mtandao huu kwa njia ya simu kuwa ameweza kufanikiwa katika ufugaji wa ng'ombe wa maziwa kwa sababu ya mapenzi yake kwa mifugo hao. "Mimi huwa sioni wakiwa na gharama ya juu kuwafuga, faida yake ni tele," alisema Bw Mathenge, ambaye ni mwalimu mstaafu wa shule ya upili.

Anaeleza kwamba kiwango cha usafi kwa ufugaji wa ng'ombe ndicho kimemfanikisha zaidi.

"Ifahamike lishe inafaa kuwa iliyokauka wala si majani mabichi. Zizi la ng'ombe lisalie safi kila mara," ashauri, maelezo yake yakionekana kuenda sambamba na ya Bi Veronicah Kirogo.

Bw Malibet asema ng'ombe wake mmoja humpa lita kati ya 20-25 kila siku, kwa kumkama asubuhi na jioni. Lita moja ya maziwa kaunti ya Kiambu hugharimu kati ya Sh60-80, hii inaonesha mfugaji huyo kwa siku na kwa kukama ng'ombe hao watatu hutia mfukoni zaidi ya Sh3, 000.

Mfugaji Matheng'e anayefichua amefanya ufugaji wa ng'ombe wa maziwa kwa zaidi ya miaka 20, asema ng'ombe wake mmoja aghalabu humpa karibu lita 30 kwa siku.

Lita moja ya maziwa Kirinyaga ni kati ya Sh50 hadi Sh70, kulingana na Bw Mathenge hasa akisisitiza hutegemea misimu ni ipi.

Kwa kutumia takwimu hizo na zaidi ya ng'ombe 10 wa kukama maziwa alio nao, inadhihirisha Bw Mathenge hupokea zaidi ya Sh15,000 kwa siku.

Kando na natija za maziwa, ng'ombe hao huwapa mbolea wanayotumia kukuza mimea na hata kuiuza. Bw Mathenge ni mkulima tajika wa kahawa na majani chai Kirinyaga na hutumia mbolea ya ng'ombe wake kutia rutuba kwenye mashamba yake ya majani chai na kahawa.

Hata hivyo, wawili hao wanateta kuwa biashara ya maziwa imeingiliwa na mawakala wanaoharibu bei ya maziwa kiasi kwamba bei wanayofaa kuuza hupata imepungua hata mara dufu.

Ombi lao kwa serikali, ni itafute njia mbadala za kuimarisha wafugaji wa ng'ombe wa maziwa hasa kwa kubuni viwanda vingi vya maziwa vitakavyokuwa vikinunua moja kwa moja kutoka kwao badala ya kutumia mawakala, wanaowakandamiza.

Serikali ya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto imekuwa ikisisitiza kwamba lengo lake kuimarisha sekta ya kilimo na ufugaji nchini, hasa kwa kuzindua mifumo ya teknolojia ya kisasa kuendesha zaraa na ufugaji.

No comments:

Post a Comment

Post Bottom Ad

Responsive Ads Here